Aliyekuwa mgombea wa urais wa tiketi ya chama cha Republican nchini
Marekani, Jeb Bush amesema hatampigia kura Donald Trump katika Uchaguzi
Mkuu utakaofanyika nchini humo Novemba mwaka huu.
Bush alisema kuwa Trump hana tabia wala mienendo ya kuwa Rais wa Marekani.
‘‘Marais wa Marekani wanasifa zao na wanakubalika kwa watu, lakini huyu
jamaa hana sifa hata moja ndiyo maana kila siku namkana na kusema hafai
kabisa kuwa rais wa nchi hii, ’’alisema Bush
Jeb ni mojawapo wa wanachama mashuhuri wa Republican kutanganza
hadharani kuwa hatampigia kura Trump kwa sababu ya kampeni yake ya
kiburi ambayo imegawanya Chama cha Republican.
Juzi Spika wa Bunge, Paul Ryan alisema hatamuunga mkono mfanyabiashara huyo tajiri ingawa atakutana naye wiki ijayo.
Hata hivyo, Trump aliungwa mkono na mgombea urais wa zamani wa nchi
hiyo, Bob Dole aliyeshindwa katika uchaguzi na Bill Clinton wa Chama cha
Democratic mwaka 1996.
Wiki iliyopita Seneta wa Texas, Ted Cruz alijitoa katika kinyang’anyiro
cha kuwania uteuzi wa kugombea urais kwa Republican baada ya kushindwa
katika uchaguzi wa awali dhidi ya mpinzani wake huyo.
Cruz aliwaambia wafuasi wake katika mji wa Indianapolis kwamba: “ Njia
hii kuelekea ushindi imefungwa” na kusema kuwa wapiga kura wamechagua
njia nyingine.
Alitoa shukrani kwa wafuasi wake wote. Trump alipata ushindi mkubwa
Indiana huku Cruz akishika nafasi ya pili na gavana wa Ohio John Kasich
akiwa katika nafasi ya tatu.
Trump alisema huo ni ushindi mkubwa kwake na kumpongeza Cruz akimuita
yeye na wagombea wengine 15 waliokuwa wanagombea uteuzi wa Republican
kuwa ni werevu na wenye nguvu.Alitoa wito wa kuwa na umoja ndani ya
chama hicho.
Kwa upande wa Democratic seneta wa Vermond, Bernie Sanders ameshinda katika jimbo la Indiana dhidi ya Hillary Clinton
Wagombea hao wawili walibadilishana ushindi kabla ya Sanders kuibuka
mshindi kwa asilimia saba ya kura. Hata baada ya ushindi huo wa Sanders
katika jimbo la Indiana, Hillary anaongoza katika idadi ya wajumbe
ikionyesha kwa mahesabu ni vigumu kwa Sanders kuteuliwa kuwa mgombea wa
Democratic
News
Monday, May 9, 2016
0 Response to " Bush Asema Hatampigia Kura Donald Trump"
Post a Comment