Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kumsimamisha
kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Dkt. Ally Yahaya Simba kutokana na
kutosimamia ipasavyo Mkataba wa utekelezaji wa mfumo wa usimamizi wa
mawasiliano ya simu (TTMS), na kusababisha nchi kupoteza mapato ya
takriban shilingi bilioni 400 kwa mwaka.
Rais Magufuli amechukua hatua hiyo leo tarehe 26 Aprili, 2016 Ikulu
Jijini Dar es salaam baada ya kufanya kikao cha kazi kati yake na
viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi,
Wizara ya fedha na Mipango na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(TAKUKURU).
Tarehe 22 Machi, 2013 Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) iliingia
mkataba na kampuni ya SGS juu ya uwekaji, uendeshaji na uhamishaji wa
mapato ya simu ambapo kampuni hiyo ilipaswa kutekeleza vipengele vitano
lakini mpaka sasa kampuni ya SGS haijaanza kutekeleza kipengele kidogo
kinachohusiana na uthibiti wa mapato ya simu za ndani (Offnet), hali
ambayo imesababisha serikali kukosa mapato yanayokadiriwa kuwa shilingi
bilioni 400 kwa mwaka.
Pamoja na kuivunja bodi ya TCRA inayoongozwa na Profesa Haji Semboja na
Kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Ally Yahaya Simba, Rais
Magufuli pia amemuagiza Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi
Profesa Makame Mbarawa Mnyaa kumteua Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka
hiyo mara moja.
Aidha, Rais Magufuli amewataka Waziri Prof. Mbarawa, Katibu Mkuu na
Naibu Katibu katika wizara hiyo kuchukua hatua mara moja ili mfumo wa
ukusanyaji wa mapato ya simu kwa simu za ndani (Offnet) uanze kufanya
kazi, na nchi ipate mapato yanayostahili kukusanywa.
“Waziri hakikisha unachukua hatua mara moja, nataka tukusanye mapato
yote ya serikali yanayostahili na sitasita kuchukua hatua dhidi ya
yoyote atakayekwamisha jambo hili” Amesisitiza Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
26 Aprili, 2016
News
Tuesday, April 26, 2016
0 Response to "Breaking Newa: Rais Magufuli Aivunja Bodi ya TCRA na Kumsimamisha Kazi Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka Hiyo Dr Ally Yahaya Simba"
Post a Comment