Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imesema tatizo la sukari nchini
limetokana na uamuzi usio sahihi wa Rais Dk. John Magufuli, kwa kupiga
marufuku uingizwaji wa bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi bila kufanya
tathmini.
Akizungumza jana na waandishi wa habari, Waziri Kivuli wa Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Anthony Komu, alisema agizo hilo
lilitolewa kwa kukurupuka na ndilo lililosababisha sukari kuadimika.
Komu ambaye pia ni Mbunge wa Moshi Vijijini, alisema kama malengo ni
kulinda viwanda vya ndani, basi lisifanyike kwa sukari pekee kwa sababu
viwanda vipo vingi na bado bidhaa zinaingia kutoka nje nchi.
Alisema kuna harufu ya upendeleo kutokana na Rais kuwa swahiba wa Rais
mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, ambaye ni mmiliki wa mashamba
ya Mtibwa, hivyo amefanya hivyo kwa kupewa ushauri mbaya huku nchi
ikiingia kwenye upungufu mkubwa wa sukari.
Alihoji kwa nini apige marufuku kwenye sukari tu wakati kuna viwanda vya
nondo, saruji na vinginevyo na vinaleta bidhaa kutoka nje.
Alisema kilichofanywa na Rais ni kukurupuka na ni kuvunja sheria.
Komu alisema kitendo cha Rais kutoa amri ya walioficha sukari
wany’ang’anywe, ni kupora haki za watu na kuua mitaji yao kibiashara.
“Hakuna sheria ambayo inaruhusu kwenda kukagua maghala ya
wafanyabiashara na kugawa bidhaa bure, hii hali hata wawekezaji
wataogopa kuja kuwekeza nchini kwa sababu wataona mazingira ya hapa
nchini ni hatarishi," alisema Komu.
Alisema serikali iandae njia mbadala ya kuwafidia watu walionyang’anywa maana wengine wamekopa kwenye taasisi za kifedha.
“Agizo la Rais lina walakini, kwani ni nani katika biashara za
watu...tunakokwenda ni kubaya kwani upungufu wa sukari ulijulikana tangu
Februari, lakini akapiga marufuku sukari kutoka nje,” alisema Komu.
Alisema katika tafiti mbalimbali ikiwamo ripoti iliyotolewa na Shirika
la BBC, mahitaji ya sukari nchini kwa mwaka ni tani 590,000, lakini
uwezo uliopo ni tani 300,000, hivyo serikali ilikuwa ni busara iruhusu
kuingizwa kwa sukari kwa sababu viwanda vya ndani vimekosa uwezo.
Alisema Rais anatakiwa kukemewa na kuambiwa kwamba anakwenda kinyume na
kwamba wao kambi ya upinzani hawatetei wanaoficha sukari, lakini
serikali itafute namna ya kukabili hali hiyo.
Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alisema taifa lina viwanda vinne
vikubwa vya sukari, lakini bado havina uwezo wa kuzalisha sukari ya
kutosha.
Alisema serikali imefanya sukari ionekane kama dawa za kulevya kutokana na kuadimika huko.
Alisema sukari hadi iletwe nchini, ni takriban wiki tano na wanaoingia
kwenye Mwezi Mtukufu wa Ramadhani watahitaji sukari kushinda vitu
vingine.
“Sisi hatutetei walioficha, lakini wamenunua ili kuuza kwa taratibu
kulingana na bei ya soko wasibughudhiwe maana kuna hatari ya benki
kushindwa kurejeshewa fedha zilizokopwa,” alisema Kubenea.
News
Tuesday, May 10, 2016
0 Response to "JE? uhaba wa sukari nchini chanzo ni Magufuli soma hapa>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>."
Post a Comment