Hatimaye uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, umevunja
mkataba wa uwekezaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam(UDA) na Kampuni
ya Simon Group Limited inayomilikiwa na mfanyabiashara, Robert Kisena.
Mkataba huo ambao umekuwa ukipigiwa kelele ndani na nje ya Serikali,
umetajwa kutokufuata taratibu za kisheria na kukiuka Sheria ya Manunuzi
(PPRA).
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, jana, Meya wa Jiji la
Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema uamuzi huo umefikiwa, baada ya
kufanyika kikao halali cha Baraza la Madiwani.
Aidha baraza hilo la madiwani pia limeamua kwamba, asilimia 51 ya hisa
zilizokuwa zinamilikiwa na kampuni hiyo zirudishwe chini ya uongozi wa
jiji hilo.
Mwita alisema madiwani walipitia upya mkataba wa uwekezaji kati ya
kampuni hiyo na Halmashauri ya Jiji, ambapo walibaini udhaifu katika
maeneo mbalimbali wakati wa makabidhiano.
Meya huyo anayetokana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na waziri mwenye dhamana
ya Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutoshirikishwa wakati wa makabidhiano.
“Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, imevunja mkataba wa makubaliano
ya kuuza Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA) kwa mfanyabiashara
Robert Kisena, baada ya kubaini kuwapo udhaifu wakati wa kuuza shirika
hili,” alisema.
Mwita alisema halmashauri ya jiji kipindi hicho, haikufuata utaratibu wa
utangazaji wa zabuni wakati wa kuuza shirika hilo, hali iliyoonyesha
wazi viongozi waliokuwa madarakani wakati huo, walikuwa na maslahi
binafsi katika kukabidhi shirika hilo mikononi mwa kampuni hiyo.
Alisema hadi sasa shirika hilo bado limesajiliwa kwa jina la Halmashauri
ya Jiji kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), hali
inayowapa nguvu ya kuvunja mkataba huo kwa sababu mmiliki wake kisheria
bado ni jiji.
“Tuliambiwa Simon Group, alikuwa anakwenda benki kuchukua mikopo kwa
hati ya Shirika la UDA, tumefuatilia benki mbalimbali tumebaini hakuna
hata hati moja ya shirika iliyowasilishwa kwenye benki kama dhamana ya
mikopo,”alisema.
Alisema shirika hilo hadi sasa lina Sh bilioni 5.9 ambazo zililipwa na
Simon Group kama malipo halali ya kuuziana shirika, jambo ambalo haliko
sawa.
“Hatuwezi kuona mikataba ya kifisadi inaendelea kuimaliza Serikali,
lazima tuchukue hatua ambazo ni pamoja na kuangalia taratibu za kisheria
ili kuivunja,’ alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, baraza hilo limeunda timu ya watu watatu
wakiongozwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee ili kuangalia athari ambazo
zinaweza kujitokeza wakati wa kuvunjwa kwa mkataba huo.
Akizungumzia hatua hiyo, Ofisa Habari wa Kampuni ya Simon Group, Deus
Bugaywa alisema hadi sasa halmashauri ya jiji haijatoa taarifa yoyote ya
kuonesha kama mkataba huo umevunjwa, licha ya magari ya UDA kuanza kazi
leo.
“Hatujapewa taarifa yoyote ambayo inasema mkataba kati ya UDA na
Halmashauri ya Jiji umevunjwa, tunaamini bado ni wana hisa halali
tutafanya kazi kwa ubia kama ulivyo mkataba wetu,”alisema Bugaywa.
Alisema kampuni hiyo, ilifuata taratibu zote za kisheria wakati wa kuingia makubaliano, wala hakukuwa na ukiukwaji wa kisheria.
Alisema kama watakabidhiwa barua ya kuvunjika kwa mkataba huo, wataangalia taratibu za kisheria ili waweze kudai haki yao.
News
Tuesday, May 10, 2016
0 Response to "Hatimae UDA yazikwa rasmi kwanini imezikwa fuatilia hapa>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>"
Post a Comment