Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), mkoa wa Dar es Salaam
kimelaani kauli iliyotolewa na Mbunge wa CCM, Goodluck Mlinga ya kuwa
ili wanawake wapate nafasi ndani ya chama hicho lazima waitwe 'baby'
neno linalo maanisha kutumiwa kimapenzi.
Hivi karibuni akichangia mjadala wa Wizara ya Katiba na Sheria Milinga
alitoa kauli hiyo iliyoibua mtafaruku Bunge hadi kusababisha wabunge wa
wanawake wa Ukawa kutoka nje ya ukumbi huo baada ya kunyimwa mwongozo na
Naibu Spika Dk Tulia Ackson.
Akizungumza jana nje ya eneo la Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH),
akiwa na viongozi wenzake walipokwenda kuchangia damu Katibu wa Chadema
Dar es Salaam Henry Kilewo alisema wamesikitishwa na kauli hiyo
ilitolewa na mbunge alipewa dhama na kuaminiwa wananchi.
Alifafanua kwamba, ili uwe mbunge wa viti maalumu ndani ya Chadema kuna
hatua nne za kupitia ikiwamo wanawake wenyewe kuchaguana ngazi ya wilaya
kupitia Baraza la Wanawake la Chadema hivyo siyo rahisi kuwa na kitu
kama hicho cha uhusiano wa kimapenzi.
"Kauli kama hizi zinapaswa kukemewa na kukomeshwa kwani zinawadhalilisha
wanawake wote Tanzania. Lakini cha ajabu nimeshangaa hata wenzetu
upande wa pili CCM wamekaa kimya bila kutoa kauli ya kukaripia," alisema
Kilewo.
Alisema Chadema mkoa wa Dar es Salaam, inaungana na wabunge wa wanawake
wa Ukawa kupinga kauli hizo za kiuni zilizotolewa na mbunge huyo wa
Ulanga Mashariki aliyepigiwa kura wananchi mbalimbali wakiwamo wanawake.
Kuhusu suala la damu Kilewo aliwataka Watanzania wote kujijengea tabia
ya kuchangia damu ili kuokoa maisha ya Watanzania wengine waliolazwa
katika hospitali na vituo vya afya mbalimbali nchini.
"Chadema Dar es Salaam, tumeonyesha mfano tunaviomba vyama vingine viige
mfano huu ili tuwasaidie watu wenye mahitaji ya damu,"alisema Kilewo.
Kwa mujibu wa Kilewo zaidi ya wanachama 40 wakiwamo viongozi wa Chadema
mkoa huo wamechangia damu na kwamba mchakato huo utakuwa kila baada ya
miezi watakuwa wakitoa msaada huo wa damu.
Kwa upande wake, Mbunge wa Viti Maalumu wa chama hicho, Ruth Molel
alisema wabunge wa viti maalumu wa Chadema wanaoteuliwa wote na
wanataalumu zao na hawabahatishi kupata nafasi hizo kama Mlinga
anavyodhani.
"Nimeumia nilivyosikia kauli hii ikitolewa na kijana yule ambaye ni kama
mwanangu, kiukweli hajatutendea kina mama. Inaonyesha jinsi gani bado
ana fikra za mfumo dume" alisema Molel.
Ofisa Habari wa MNH,Neema Mwangomo alisema kwa siku hospitali hiyo
inahitaji damu kwa wastani uniti 80 hadi 100 lakini zinazopatikana ni
40.
Hata hivyo, Mwangomo aliwashukuru viongozi Chadema kwa moyo wao na
kuwataka Watanzania wengine kujitokeza kutoa damu katika hospitali hiyo
News
Saturday, May 7, 2016
0 Response to " Chadema Walaani Kitendo cha Udhalilishaji Bungeni Walichofanyiwa Wabunge wa Wanawake wa Ukawa"
Post a Comment