Chama cha Alliance for Democratic Change ADC kimewafuta uanachama
wanachama wake wanne akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Bwana Said
Miraaj,Katibu Mkuu Bi.Lydia Bendera,Mkurugenzi wa mipango na uchaguzi
Bwana Jumanne Magafu pamoja na Katibu wa Kamati ya ulinzi Bwana Juma
Wandwi kwa makosa ya kukiuka katiba ya chama hicho kwa kususia kushiriki
uchaguzi mkuu wa marudio wa Zanzibar.
Maamuzi hayo yamefikiwa katika mkutano mkuu wa chama hicho ambapo
akizungumza baada ya ufunguzi aliyekuwa mlezi wa chama cha ADC ambaye
pia ni Waziri wa Kilimo Zanzibar,Mhe.Hamad Rashid amesema katiba ya
chama inasisitiza ushiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za
uongozi,hivyo kutoshiriki ni kukivunja nguvu chama katika mikakati yake
ya kuchukua dola.
Akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa -ADC- Msajili Msaidizi wa
vyama vya siasa Bwana Sisty Nyahoza amesema kitendo cha chama cha siasa
kutoshiriki uchaguzi kinakwenda kinyume na sheria ya vyama vya siasa na
malengo ya kuanzishwa chama Chochote cha siasa na kusisitiza ipo haja ya
kuangalia mfumo wa usajili wa vyama utakaowezesha kutoa adhabu kwa
vikavyoonekana kukataa kushiriki katika chaguzi.
Aidha katika mkutano mkuu huo, wajumbe wamemchagua aliyekuwa mlezi wa
ADC ambaye kwa sasa ni Waziri wa Kilimo Zanzibar Mhe.Hamad Rashid kuwa
mwenyekiti wa chama hicho taifa na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa chama
hicho Bwana Doyo Hassan Doyo amechaguliwa kushika wadhifa wa katibu mkuu
wa chama.
News
Sunday, May 8, 2016
0 Response to "ADC Yawafuta Uanachama Wanachama wake Wanne Akiwemo Mwenyekiti wa Chama hicho Said Miraaj kwa Kususia Uchaguzi mkuu wa Marudio wa Zanzibar"
Post a Comment