Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amesema hatua
anazochukua kwa ajili ya kuwasimamisha watumishi wa umma kazi
zisitafsiriwe kama ni ukatili kwakuwa watumishi hao wamekuwa wakifanya
mambo kinyume na maadili ya utumishi wa umma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo
tarehe 08 Mei, 2016 ameungana na waumini wa Parokia ya Toleo la Bwana
iliyopo katika Jimbo Katoliki la Arusha kusali ibada ya Jumapili, ambapo
katika salamu zake amewaomba watanzania kuendelea kuiombea nchi yao ili
kazi anayoifanya ya kukabiliana na matatizo yanayowakabili watanzania
wanyonge ifanyike kwa mafanikio.
Dkt. Magufuli amesema hayo alipokaribishwa na Mwenyekiti wa Parokia hiyo
Bw. Philemon Mushi kuwasalimu waumini wa kanisa hilo, mara baada ya
kumalizika kwa ibada ya Jumapili ya kupaa kwa Bwana.
"Niko pamoja na nyinyi ndugu zangu watanzania na wana Arusha wote,
napenda kuwaahidi tena sitawaangusha, nitasimama mbele kuwatetea
masikini, siku zote nitakuwa upande wenu, siku zote nitatembea na
nyinyi, nasema kwa dhati kabisa na nataka muamini hilo kwamba
sitawaangusha" amesema Rais Magufuli huku akishangiliwa na waumini
walioshiriki ibada hiyo.
Rais Magufuli amewahakikishia watanzania wote kuwa atahakikisha ahadi
zote alizoziahidi anazitekeleza na amewaomba watanzania wote kuungana na
kushikamana ili kufanikisha juhudi za kuijenga Tanzania bora.
"Ninajua kuongoza ni kazi kubwa, ninajua kuongoza Taifa lililo masikini
kama Tanzania inahitaji mkono wa Mungu, kwa hiyo niwaombe sana ndugu
zangu Wakristo na watanzania kwa ujumla, muendelee kuliombea Taifa hili,
kuniombea mimi, na pia kujiombea sisi wote ili amani tuliyonayo katika
nchi yetu iendelee kudumu katika maisha yote.
"lakini siku zote katika matendo yetu kila tunapofanya tumtangulize
Mungu kwa sababu Mungu ndio kila kitu, lakini tutambue kwamba siku moja
tutakufa, kwa hiyo ni vyema katika matendo yetu tutakapokuwa hapa
duniani tujitahidi sana kufanya matendo mazuri kwa ajili ya watu na hasa
watu wanyonge, ambao kwa kweli watanzania waliowanyonge wanapata shida
sana" Amebainisha Rais Magufuli.
Pia Dkt. Magufuli amewasihi watanzania wote kuachana na ushabiki wa
vyama vya siasa na badala yake waungane katika ujenzi wa Taifa na
kukabiliana na kero zinazowaumiza
News
Sunday, May 8, 2016
0 Response to "Utumbuaji Majipu Siyo Ukatili- Rais Dkt. Magufuli Afunguka Kanisani"
Post a Comment