Thomas Ulimwengu Afunguka Pengo la Samatta bado lipo TP Mazembe

blogger templates
Mshambuliaji wa kimataifa Thomas Emmanuel Ulimwengu amesema kwamba kwa sasa pengo la Mtanzania mwenzake, Mbwana Ally Samatta linaonekana TP Mazembe.

Ulimwengu akiongea na Clouds FM alisema TP Mazembe kwa sasa inamkosa mshambuliaji mwepesi, mwenye uwezo wa kufunga kama Samatta.

Samatta ameondoka timu hiyo ya DRC Januari mwaka huu baada ya kushinda nayo taji la Ligi ya Mabingwa Afrika na kujiunga na KRC Genk ya Ubelgiji anakoendelea vizuri hivi sasa.

Tangu kuondoka kwa Samatta, Mazembe imeonekana kupoteza makali yake kiasi cha kuvuliwa mapema ubingwa wa Afrika.

Mazembe ilitolewa na Wydad Casablanca ya Morocco katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa na kuangukia kwenye kombe la Shirikisho.

Katika mechi iliyopita Mazembe ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika dhidi ya Stade Gabesien Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi.

Ulimwengu aliyecheza kwa dakika 45 juzi kabla ya kutoka uwanjani akiwa anachechemea, alisema timu kwa sasa haina mtaalamu wa kufunga mabao kama alivyokuwa Samatta.

“Pengo la Samatta linaanza kuonekana sasa, pale mbele hakuna na anayeweza kufunga kama Samatta, tunapoteza nafasi nyingi sana, hilo ndilo tatizo,”amesema Ulimwengu.

Sasa Mazembe itakuwa na kazi ngumu katika mchezo wa marudiano wiki ijayo, ikitakiwa kwenda kuulinda ushindi huo mwembamba nchini Tunisia

0 Response to "Thomas Ulimwengu Afunguka Pengo la Samatta bado lipo TP Mazembe"

Post a Comment