Shehena ya sukari ya kilo milioni 34 zilizokuwa zimefichwa kwenye
maghala ya wafanyabiashara watatu Kilimanjaro imekamatwa na vyombo vya
usalama, na serikali mkoani humo imetangaza kuiuza kwa wananchi kuanzia
jana kwa bei elekezi ya Sh. 1,800.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecki Sadiki alithibitisha jana
kukamatwa kwa shehena hiyo, baada ya makachero wanaoongoza timu maalumu
ya ukaguzi wa maghala ya wafanyabiashara na mawakala wa sukari kubaini
kufichwa kwa bidhaa hiyo.
“Tumefanya ukaguzi katika maghala 45 na katika harakati hizo tumenasa kilo milioni 34 za sukari iliyokuwa imefichwa," alisema.
"Katika zoezi hilo kuna mfanyabiashara mmoja mkubwa, yeye alikutwa na
tani 31.33 lakini alikuwa akiiuza, isipokuwa bado tumewapa kazi Mamlaka
ya Mapato (TRA) ichunguze kama imehodhiwa isivyo halali,” alisema
Sadiki.
Kiasi cha sukari iliyobakia, alisema Mkuu wa M koa huyo, kilikamatwa kwa
wafanyabiashara wengine wawili, ambao walikuwa na tani nne kasoro,
Moshi mjini na Marangu.
Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa mkoa, shehena hiyo ya sukari hadi jana mchana
ilikuwa ikishikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kukamilisha
taratibu za kiuchunguzi na kwamba ametoa amri igawiwe kwa wananchi kwa
bei elekezi iliyotangazwa na serikali.
Kuhusu upungufu wa sukari Kilimanjaro, Sadiki alisema "Sisi kama mkoa
tumefanya mawasiliano na mawakala walioko Dar es salaam, ambao sukari
yao ilikuwa inashikiliwa na vyombo vya usalama na wametuahidi kuukabili
uhaba wa sukari uliopo hapa kwetu.
“Jana (juzi) niliwasiliana na Mmiliki wa Kampuni ya Zakaria Enterprises
na amekubali kuwapa bidhaa hiyo mawakala ambao ni wadau wa Kiwanda cha
Sukari cha TPC," alisema Sadiki.
"Kwa hiyo tunakwenda vizuri na tumejipanga kuhakikisha kwamba uhaba huo
tunaupatia ufumbuzi wa kudumu.Ila ninawaomba wananchi wangu wawe
wavumilivu kwa sasa.
"Mawakala wakubwa wa sukari wa Kilimanjaro na mikoa ya Kanda ya
Kaskazini ni mfanyabiashara Vicent Laswai ambaye atapatiwa tani 600 za
sukari kutoka Kampuni ya Zakaria, alisema Mkuu wa Mkoa huyo.
Aidha, Laswai atapokea tani 640 toka katika Kampuni ya Mohamed Enterprises, alisema.
Kampuni ya Zakaria pia imekubali kutoa tani 640 kwa Kampuni ya Marenga
Investment, alisema Sadiki na kubainisha kuwa Mohamed Enterprises
imemuahidi kuziba pengo la upungufu utakaojitokeza.
Tangu Rais Magufuli apige marufuku uingizaji sukari kutoka nje ya nchi
Februari 17 mwaka huu, baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu
wamekuwa wakificha bidha hiyo kama njia ya kuihadaa serikali kwamba kuna
uhaba mkubwa.
Wakati akipiga marufuku, Magufuli alisema kama kutakuwa na uhitaji wa
sukari kuingia nchini, vibali atavitoa yeye si mtu mwingine yeyote ili
kuviwezesha viwanda vya ndani viendelee kuzalisha bidhaa hiyo, kuendelea
kutoa ajira na kuinua kipato cha wakulima wa miwa.
Alisema inasikitisha kuona sukari ikiingizwa nchini kutoka nje wakati
nchi ina viwanda vingi vya bidhaa hiyo na kusababisha Watanzania wengi
kupoteza ajira kutokana na sukari wanayozalisha kukosa soko.
"Nakuagiza Waziri Mkuu, kuanzia leo, marufuku mtendaji yeyote wa
Serikali kutoa kibali cha kuagiza na kuingiza sukari kutoka nje ya
nchi...vibali vyote nitatoa mimi," alisema Rais Magufuli.
"Katika kampeni zangu mwaka 2015, nilisema Serikali yangu itakuwa ya
viwanda hivyo lazima tuvithamini viwanda vya ndani na kulinda bidhaa
zinazozalishwa."
News
Sunday, May 15, 2016
0 Response to "Serikali Yanasa Kilo 34,000,000 za Sukari Mafichoni"
Post a Comment