Sakata la upotevu wa vifaatiba na dawa kutoka Bohari ya Dawa (MSD)
kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kipindi cha miaka minne
limeingia katika sura mpya baada ya MSD kuigeuzia kibao hospitali hiyo,
huku ikitoa ushahidi wa ankara 23 zilizotumika kupelekea vifaa hivyo kwa
kipindi cha miaka minne.
Ripoti iliyotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Profesa Mussa Juma Assad inaonyesha ukaguzi ulifanyika Muhimbili,
huku rekodi zikionyesha kwamba hospitali hiyo ilikuwa ikiagiza mzigo
kutoka MSD, lakini hazionyeshi kupokea vifaa hivyo tangu mwaka 2012/14.
Kwa kutumia vielelezo vya nyaraka hizo mbele ya vyombo vya habari jana,
MSD ilitoa ufafanuzi kuwa haihusiki katika upotevu huo kwani
iliwasilisha MNH vifaatiba na dawa zenye thamani ya Sh2.6 bilioni na
kupokewa stoo kwa nyakati tofauti kwa kipindi cha miaka minne.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Lauren Bwanakunu alisema hati za CAG, zinaonyesha kuwa MSD haina tatizo lolote.
“Ankara hizo siyo kwamba dawa hazikufika hospitalini hapo, bali
hazikuonekana kwenye vitabu vya kupokelea mali vya Hospitali ya Taifa
Muhimbili,” alisema.
Alisema baada ya kupitia nyaraka zake, MSD imefanikiwa kupata
uthibitisho wa hati za kupelekea mali za dawa na vifaatiba vyote
vilivyopelekwa Muhimbili, ambavyo ni pamoja na dawa za figo na moyo.
Bwanakunu alisema pamoja na juhudi hizo, Bohari ya Dawa imewasiliana na
Muhimbili ili kuainisha taarifa za kwenye ankara na shehena ya dawa na
vifaatiba vilivyopelekwa hospitalini hapo, kwani utaratibu wa kupeleka
na kukabidhi dawa hospitalini unamlazimu mpokeaji kusaini ankara
inayoonyesha mzigo uliopelekwa kwa mteja (delivery notes) ambazo zote
zipo Bohari ya Dawa.
“Vitabu vyetu kutoka kwa CAG vipo na tumepata hati safi, tumethibitisha
kwamba mzigo wote wa ankara 23 ulipelekwa Muhimbili kwa kipindi cha
miaka minne,” alisema.
Alisema MSD ilikuwa ikiwasilisha dawa tangu mwaka 2012 kwa mujibu wa
maombi kutoka MNH, hivyo hospitali hiyo inapaswa kujibu kwa kuwa imekuwa
ikipokea dawa hizo kwa kipindi tofauti.
“Vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh2.03 bilioni vilikuwa vikiagizwa kwa
tarehe tofauti kwa miaka mitatu lakini havikuwahi kuingizwa katika
rekodi.
"Kulingana na utaratibu wa usambazaji wa MSD, mteja hukiri kupokea mzigo
kupitia Ankara ya mauzo (Sales Invoice), jukumu la kuandika hati ya
mapokeo (GRN) ni la mteja husika ambaye ni Muhimbili,” alisema Bwanakunu
huku akionyesha nakala hizo.
Ankara zilizotolewa jana na MSD zinaonyesha kuwa ilikuwa ikihudumia
hospitali hiyo tangu Mei 14, 2012 hadi Desemba 4, 2014, lakini katika
ankara hiyo, Muhimbili haikuonyesha kuwahi kupokea vifaa hivyo vyenye
thamani ya Sh2,028,625,100.
Alichosema CAG
Katika ukurasa wa 37, taarifa ya CAG, inaeleza kuwa ukaguzi huo ulibaini
kuwa dawa na vifaatiba vyenye thamani ya Sh2.03 bilioni havijafika
Muhimbili tangu Mei 2012 licha ya kuonekana kwenye ankara 23 za MSD.
Nakala hiyo ilieleza kuwa kwa hali ya kawaida, haikutarajiwa bidhaa hizo
kuchukua zaidi ya wiki moja kufikishwa sehemu husika ukizingatia ofisi
za MSD na MNH zote zipo Dar es Salaam.
“Hali hii inaashiria uwezekano wa upotevu wa dawa na vifaatiba pasipo
uongozi kuwa na taarifa. Menejimenti inashauriwa kuchunguza jambo hili
ili kubaini kama kweli bidhaa hizo bado zipo safarini,” inasema taarifa
ya CAG.
Msimamo wa Muhimbili
Akijibu hoja hiyo Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma, Hospitali ya
Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema MNH inazo hati za kupokelea
‘Develivery note’ za mizigo iliyopokea bila ankara, kinachohitajika ni
MSD kuoanisha ankara walizozitaja na hati walizozifikisha hospitalini
hapo.
Aligaesha alisema namba za ankara zilipatikana kwenye maelezo ya MSD
yaliyowasilishwa MNH ikionyesha matumizi ya hospitali kwenye akaunti
iliyopo MSD kutokana na fedha ambazo Serikali inapeleka huko.
“Ili kukamilisha utaratibu wa kupeleka mzigo mahali, mzigo huo unapaswa
uambatane na nyaraka kama mkataba kati ya mnunuaji na muuzaji, ankara na
hati ya kupokelea. Endapo mzigo ulioletwa ni wa msaada, mkataba
hauhitajiki, kwenye msaada ni lazima hati ya kupokelea iwepo na nakala
inayoonyesha thamani ya mzigo,” alisema.
Alisema kwa muda mrefu imekuwa ni kawaida MSD kupeleka baadhi ya mizigo
Muhimbili au wazabuni walioagizwa na MSD ikiwa haina viambatanisho hivyo
muhimu, kwani mpaka sasa Muhimbili ina orodha ya mali ambazo
zilipelekwa kwa kutumia hati ya kupokelea katika kipindi husika.
“Hata hivyo, tulifuatilia ankara za mizigo iliyokwishapokewa kutoka MSD
ili tuweze kupewa ankara husika kwa mizigo tuliyopokea bila
kiambatanisho hicho, lakini kwa bahati mbaya ankara zilizodurufiwa
kutoka kwenye mfumo wa MSD hazionyeshi namba ya hati (customer
reference) na hazijasainiwa na wao wala sisi,” alisema Aligaesha
News
Saturday, April 30, 2016
0 Response to "MSD Yaigeuzia Kibao Muhimbili Kuhusu Kuhusu Utata wa Dawa Uliobuliwa na CAG"
Post a Comment