Na Raymond Mushumbusi – MAELEZO
Utafiti uliofanyika hivi karibuni na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) umebaini kwamba asilimia 71 ya watanzania wanatumia muda mwingi kufanya shughuli zisizokuwa za uzalishaji mali wala tija binafsi kwao na Taifa kwa ujumla.
Akizundua taarifa ya utafiti huo leo jijini Dar es salaam Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera,Bunge,Kazi,Ajira,Vijana na watu wenye ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa idadi hiyo hufanya kazi zisizoleta tija kwao na taifa na muda mwingi huutumia kujihudumia binafsi kwa kulala na starehe nyingine.
Ameeleza
kuwa takwimu hizo zinaonesha wazi ni kwa namna gani watanzania
wanashindwa kujishughulisha katika kufanya kazi zenye kuwaingizia kipato
na badala yake wanatumia muda wao mwingi kufanya shughuli zisizo za
uzalishaji hasa kufanya starehe mbalimbali.
“Ndugu
zangu watanzania unakuta mtu amekaa baa au anacheza “poll table”
kuanzia asubuhi mpaka jioni na hujui anafanya kazi gani ya uzalishaji,
ndugu zangu tuone aibu basi tujishughulishe tulijenge taifa letu ili
kujiletea maendeleo yetu na nchi yetu.”
Aidha,
matokeo hayo yamebainisha kuwa asilimia 18.5 ya wananchi wanafanya kazi
za uzalishaji na asilimia 10.6 ni wale wanaofanya shughuli za nyumbani
zisizo na malipo huku uchambuzi wa kijinsia ukionesha kuwa wanaume
asilimia 23.8, wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za kiuchumi
ikilinganishwa na asilimia 13.5 ya wanawake.
Amefafanua
kuwa wanawake ambao ni asilimia 16.5 katika utafiti huo wanatumia muda
mwingi kufanya kazi za nyumbani zisizo na malipo ikilinganishwa na
asilimia 4.4 ya wanaume.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisa ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt.
Albina Chuwa amesema kuwa upatikanaji wa Takwimu hizo utaisaidia
Serikali kupata mbinu sahihi za kuondokana na tatizo la ajira nchini kwa
kuunganisha nguvu kutoka sekta isiyo rasmi ili kuleta changamoto katika
soko la ajira nchini.
Amesema
kuwa hii ni mara ya tano Tanzania inafanya utafiti huo na kubainisha
kuwa ulianza mwezi Januari hadi Desemba, 2015 ukitumia sampuli ya
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 iliyotumika kupata taarifa sahihi
ya takwimu hizo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira na Wenye Ulemavu),Jenista Mhagama,akizindua ripoti ya matokeo ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2014 katika Viwanja vya Karimjee,Dar es Salaam. Wengine wanaoshuhudia ni kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa Takwimu nchini,Dk.Albina Chuwa, Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu za Jamii,Ephraim Kwesigabo na Mwakilishi kutoka Shirika la Kazi Duniani,Marry Kawar.
0 Response to "Asilimia 71 Ya Watanzania Hawataki Kufanya Kazi"
Post a Comment