Wakati aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC),
ametajwa kutenguliwa uteuzi wake kwa kukataa kuchukua mshahara wa
Serikali kwa miaka mitatu mfululizo, uchunguzi umebaini kuwa jipu la
kusamehe kodi Kampuni ya Saruji ya Dangote ndilo lililomwondoa.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa mbali na Juliet Kairuki kutochukua
mshahara wa Sh 5,000,000 kila mwezi aliopangiwa na Serikali kwa miaka
mitatu, kwa maana kuwa ameacha kuchukua wastani wa Sh milioni 180 kwa
muda huo, anatuhumiwa kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa
wawakezaji bila kufuata utaratibu au sheria za nchi.
“Hili la mshahara ni cha mtoto. Amewadanganya wawekezaji wengi kuwa
anaweza kuwapa msamaha wa kodi ya VAT, na sasa Serikali hii ilipoingia
madarakani ikasema hana mamlaka hayo. Mwekezaji wa kwanza aliyedanganywa
ni Dangote,” anasema mtoa taarifa wetu.
Uchunguzi uliofanywa umebaini kuwa Novemba, 2015 Kampuni ya Dangote
iliingiza nchini makaa ya mawe tani 35,000 kutoka Afrika Kusini na
kutaka makaa haya yasamehewe kodi zote.
“Kwa kweli tulishangaa sana. Kwanza, makaa ya mawe si bidhaa za mtaji
(capital) bali ni za matumizi tu (consumables). Vifaa vinavyosamehewa
kodi ni zile zinazotumika kuzalisha bidhaa nyingine leo, kesho, mwakani
au miaka mitano ijayo na kuendelea, ila makaa ya mawe ukiyachoma
yanaisha siku hiyo hiyo, hivyo hii si mtaji.
“Ukiacha hilo, hawa watu wa Dangote wameambiwa wanunue makaa ya mawe
kutoka Kiwira au Ngaka, lakini hawataki,” kinasema chanzo chetu na
kuongeza kuwa kwa mwaka uliopita, waliagiza tani 2,000 tu za makaa ya
mawe kutoka Tancoal kinyume cha makubaliano ya kuongeza ajira nchini.
Afisa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) amefichua katika uchunguzi
huu kuwa kinachoendelea kwenye Kampuni ya Dangote ni balaa. “Hii
kampuni tulidhani imekuja hapa kukomboa wananchi, lakini uhalisia siyo.
“Kampuni hii inafanya malipo bila kutoa kodi ya zuio, bidhaa inazoingiza
nchini pamoja na nyingine kupata misamaha ya kodi bado inaongeza bei
zinakuwa ghali mno kwa maana ya kuongeza gharama za uzalishaji na hivyo
kupunguza kiasi cha kodi kinachostahili kulipwa… ni shida,” anasema
afisa huyo kwa uchungu.
Kutokana na mkanganyiko huo, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania
(TRA), Alphayo Kidata, ameunda timu ya kufanya ukaguzi maalumu kwa
Kampuni ya Dangote ambayo imewakuta na hatia.
“Hiyo bilioni 20 ni uchunguzi wa awali, tunaweza kupata kiasi kikubwa
zaidi. Tunawashukuru kwa kuandika habari za ukwepaji kodi, na
nakuhakikishia sisi tunafuatilia kila mnachochapisha,” anasema mtoa
habari wetu.
Afisa mwingine wa TRA anasema mbinu kubwa inayotumiwa na Dangote na
kampuni nyingine ambazo tayari TRA imekwishaibaini mbinu wanazotumia
kupunguza faida (Tax Base Erosion), kwa kuingia mikataba yenye gharama
kubwa na kampuni walizo na uhusiano nazo kibiashara, kuonesha wametumia
gharama kubwa wakati uhalisia wanafanya mbinu za kukwepa kodi.
Akizungumzia sakata hili, Mejena Mkuu Mwandamizi wa Kampuni ya Dangote,
Vidya Dixit, amekiri kupokea ankara ya malipo kutoka TRA yenye thamani
ya bilioni 20 na akasema: “Wakaguzi wa TRA wako hapa, wamefanya
uchunguzi wao, wametuletea madai yao, na sisi tunawasiliana na mshauri
wetu wa masuala ya kodi, ikithibitika kuwa tunadaiwa kiasi hicho Dangote
ni kampuni kubwa, tutalipa.”
Dixit amesema TRA wamekagua mikataba mbalimbali wanayotumia akina
Dangote kuagiza bidhaa na huduma, na wakaja na kiasi hicho, hivyo kwake
halioni kama ni tatizo, washauri wao wa masuala ya kodi wakikuta ni
kweli watalipa tu. Chanzo chetu kimetueleza kuwa mshauri wao ni Kampuni
ya PriceWaterhouseCoopers (PWC) ya Afrika Kusini.
Meneja huyo alijibu pia swali kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TRA) inawadai dola 2,867,400 za Marekani (sawa na Sh bilioni
6.3), kwa kusema: “Mimi sisimamii idara ya uhasibu. Madeni hayo yanaweza
kuwapo, ila Dangote ni kampuni kubwa, kama kuna madeni ya aina yoyote
tutalipa tu baada ya kujiridhisha kuwa ni madeni halali.”
Kuhusu suala la tani 35,000 za makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini,
alisema wao kama Dangote hawapaswi kulaumiwa kwani walifuata taratibu
zote: “TIC walitupa sisi msamaha wa kodi, sasa tumezungumza na Waziri wa
Fedha akasema TIC hawana mamlaka ya kutoa msamaha wa kodi bila
kutangaza kwenye Gazeti la Serikali (GN) na kweli hakukuwapo GN yoyote.
“Sasa hapa tunapata tabu kidogo, idara moja ya Serikali inasema hivi na
idara nyingine inasema vile, tunapata shida kidogo,” anasema Dixit.
Katika makaa hayo ya mawe pekee ambayo wanatakiwa kuyanunua kutoka
nchini, Dangote wanadaiwa wastani wa Sh bilioni 1.1.
Kuhusu tuhuma zinazoelekezwa kwa kiwanda hicho kuwa kimewageuka
wafanyabiashara wadogo na kupendelea wafanyabiashara wakubwa kwa njia ya
kuwauzia saruji nyingi na kutowajali wadogo, Dixit anasema wao hawana
ubaguzi na ucheleweshaji unaweza kutokea kunapotokea dharura.
Anasema kuna wakati wanaangalia nani ana ghala kubwa la kuhifadhia
saruji kiasi gani, ila hiyo haiondoi ukweli kwamba hawabagui yeyote
anayetaka kununua na kuuza saruji ya Dangote.
“Ukisema kuna walioshindwa kupata saruji kwa wiki moja au mbili, hilo
naweza kukuelewa, lakini miezi miwili, wala asikudanganye mtu. Hilo
haliwezekani. Ni kweli kule Lindi tunakotoa chokaa, machimbo yote kwa
siku tatu zilizopita yalijaa maji, tukashindwa kupata chokaa, lakini
zaidi ya hapo kila mtu anapewa fursa sawa ya kununua saruji bila
ubaguzi,” anasema Dixit.
Awali, baadhi ya wafanyabiashara waliilalamikia Kampuni ya Dangote kuwa
inauza saruji kwa upendeleo, hali inayowafanya wakose mapato kwani
wamekopa mikopo benki na wanaishia kutopata saruji kwa wakati hivyo
wanashindwa kulipa hiyo mikopo.
“Kuna mfanyabiashara ameweka kwenye akaunti ya Dangote Sh bilioni 2.5,
huyu ndiye anayepewa saruji sisi wengine tunapuuzwa. Watanzania wengi
wamekopa benki wastani wa Sh milioni 20, 30 au 50 wanaziweka kwenye
kampuni ya Dangote na hawapati hiyo saruji. Hii inatutia hasara mno.
Tunataka usawa katika biashara hii,” anasema mmoja wa wafanyabiashara
anayedai ameweka Sh milioni 25 kwenye Kampuni ya Dangote, lakini
hapatiwi saruji.
Pia, wanalalamikia bei kubwa ya saruji ya Dangote kwani wakati kiwanda
kinaanza kujengwa Watanzania walitangaziwa kuwa mfuko mmoja wa saruji
ungeuzwa kwa Sh 8,000, lakini sasa bei inafikia Sh 16,000 kwa mikoa kama
Mwanza na kwa Dar es Salaam inauzwa kati ya Sh 10,800 na 12,500.
Kamishna Mkuu wa TRA, Kidata, hakuwa tayari kulizungumzia kwa undani
suala la Dangote zaidi ya kusema: “Hili suala lipo, tunalifanyia kazi,
ni mapema mno kulizungumzia kwa sasa.”
Hata hivyo, afisa mwingine mwandamizi alishangaa kusikia kuwa Dangote
bado wanatafuta ushauri wa kisheria kama walipe kodi hiyo au la: “Hawa
waliishakwenda hadi kwa Bwana Mkubwa wakakubali kulipa, sasa leo
inakuwaje wanatafuta ushauri?” Alihoji afisa huyo.
Alichosema ni kuwa kila mfanyabiashara mkubwa kwa mdogo ajiandae kulipa
kodi. “TRA haitaingilia mapato halali ya mfanyabiashara yeyote, ila kwa
yeyote anayekwepa kodi hili halitavumiliki. Serikali ya sasa inasema
hapa ni kazi tu, hakuna habari ya jina kubwa au dogo. Jipu ni jipu tu,
bila kujali ni kubwa au dogo, yote yatakamuliwa tu.
News
Friday, May 6, 2016
0 Response to " Mfanyabiashara Dangote Atajwa Kutumbuliwa kwa Juliet Kairuki TIC"
Post a Comment