Mahakama Kuu jijini Nairobi imeamua
kwamba Kifungu cha Sheria ambacho kimekuwa kikitumiwa kuwafungulia
mashtaka watu kuhusiana na ujumbe kwenye simu na mitandao ya kijamii
Kenya ni haramu.
Jaji wa Mumbi Ngugi alisema kifungu hicho, cha kutumia vibaya kifaa cha mawasiliano, kinakiuka katiba.Kifungu hicho nambari 29 katika Sheria ya Habari na Mawasiliano Kenya Nambari 3 ya 1998 hupendekeza faini ya Sh50,000 au kifungo cha miezi mitatu jela, au adhabu zote mbili, kwa mtu anayepatikana na hatia.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) na Mwanasheria Mkuu walikuwa wametetea sheria hiyo wakisema ililenga kulinda sifa za wengine.
Jaji Ngugi alisema maelezo ya kifungu hicho ni mapana sana na pia baadhi ya makosa yanayolengwa kwenye kifungu hicho yameangaziwa katika sheria nyingine.
Aidha, alisema hakijatimiza matakwa ya Kipengele 24 cha Sheria ambacho kinaeleza ni katika hali gani ambapo haki za kimsingi zinaweza kubanwa. Aidha, alisema kifungu hicho kinakiuka Kipengele nambari 33 cha Katiba.
“Iwapo lengo ni kulinda sifa za watu wengine, basi hilo limeangaziwa kwenye sheria ya kuwaharibia sifa watu wengine,” Jaji Ngugi alisema kwenye uamuzi wake.
0 Response to "Mahakama yatupa 'sheria ya matusi' mtandaoni Kenya"
Post a Comment