Wakazi wa Kijiji cha Nala na vitongoji vyake juzi walimpelekea maji
machafu Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na
Walemavu Anthony Mavunde wakimtaka ayanywe kwa kuwa ndiyo wanayotumia.
Mavunde alikutana na mkasa huo muda mfupi alipoingia kwenye kijiji hicho
umbali wa kilomita tisa nyakati za jioni, ambako wakazi wa eneo hilo
walikuwa wakimsubiri tangu asubuhi.
Mama mmoja aliyekuwa eneo hilo, alifika na chupa ya maji akimtaka Naibu
Waziri ayaonje mbele yao, kwani nao ni binadamu kama yeye na
wanayatumia, lakini Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Paul
Luhamo alimzuia kuyanywa.
Pamoja na taarifa ya kijiji iliyotolewa na Ofisa Mtendaji wa Kata,
Mathias Ndologa, wakazi hao walilipuka na kupiga kelele wakiipinga
taarifa hiyo kwamba iligusa kwa juu matatizo yao, lakini ikaacha jambo
kubwa la maji.
Kwenye risala yake, Ndologa alikuwa ameelezea suala la maji, umeme,
miundombinu na upungufu wa madawati, lakini kelele zilizidi kutoka kwa
wananchi wakisema jambo la msingi kwao ni moja tu, yaani maji.
Muda mfupi kelele zilianza watu wakitaka kuuliza mambo waliyoyaita ni ya
msingi, ndipo Mavunde akaamuru wapewe nafasi ya kuuliza kwanza kabla
hajasimama kuwasalimia.
Mmoja wa wauliza maswali alikuwa Daudi Lusinde, ambaye alieleza namna
wakazi wa kijiji hicho wanavyopata adha kubwa katika kutafuta maji
ambayo aliyaita ni kama dhahabu kwao.
Lusinde alisema wamepata tabu hiyo kwa muda mrefu na bado hawajaona
mwanga wa matumaini zaidi ya kuendelea kuumia huku ndoo ya maji ikifikia
bei ya Sh500.
“Bei ya sukari inapanda kila kukicha, lakini siyo shida hapa tatizo ni
maji, mheshimiwa sisi tunanunua maji kwa gharama kubwa na ukishindwa
kiasi hicho unalazimika kuchangia maji na mifugo sijui kama tutapona,”
alisema Lusinde na kusababisha mkutano kulipuka kwa shangwe.
Uongozi wa kijiji na chama wilaya ulizuia kelele za vijana waliomtaka
mbunge huyo aende hadi maeneo wanayochota maji akajionee, ikiwamo uchafu
wa maji pamoja na umbali wake.
Akijibu hoja hizo, Mavunde alieleza kusononeshwa na kuahidi kuanzia leo
ataanza kutekeleza ahadi yake hiyo kabla ya kufanya jambo lolote.
“Kwa kweli maji ni moja ya ahadi nilizoahidi kwenu, kesho ni Jumapili
siyo siku ya kazi, lakini kuanzia keshokutwa (Jumatatu) nitaleta hapa
wataalamu kuanza kuchimba kisima kwa gharama zangu,” alisema Mavunde.
Huku akiwa amesimama na maji aliyopewa, alisema yuko tayari kuacha
shughuli za Bunge akashirikiane nao kuhangaikia maji, hadi pale
watakapoyapata na kuanza kujenga matangi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo, Naibu Waziri
alisema katika kipindi cha kampeni alifika eneo hilo na kuahidi
kuwapatia maji, lakini muda ulikuwa bado. Hata hivyo, Serikali ya awamu
ya tano ina miezi sita madarakani.
“Hiyo ilikuwa ni sehemu ya ahadi yangu kwenye kampeni, kwa hiyo matatizo
ya maji hapa nayajua na kweli ni makubwa, ndiyo maana nimeamua kuvuruga
kila ratiba ili niokoe watu hawa kweli wako kwenye mateso,” alisema.
Mhandisi wa Maji Manispaa ya Dodoma, Simon Sasala alisema kijiji hicho
kina wakazi 7,600 ambao wanahitaji lita 230,000 za maji kwa siku, lakini
kuna kisima kinachotoa lita 89,000 na wakati mwingine hakifanyi kazi.
Sasala alisema maji hayo hayatoshelezi kwani yapo kwa asilimia 39, hali
ambayo inawapa shida hasa kina mama kutokana na wengi wao kulazimika
kufuata maji ya kutumia umbali mrefu.
News
Monday, May 9, 2016
0 Response to "Naibu Waziri Anthony Mavunde Apewa Maji Machafu na Wapiga Kura Wake Ili na Yeye Ayanywe"
Post a Comment