Mbunge Apewa Siku 3 Atoe Ushahidi wa Magari 777 ya Washawasha

blogger templates
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amempa siku tatu Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (Chadema) awasilishe mbele ya Kamati ya Maadili ya Bunge, maelezo ya utetezi dhidi ya madai aliyotoa bungeni kuhusu Serikali kununua magari ya washawasha 777.

Ndugai alitoa amri hiyo kutokana na mwongozo ulioombwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni juzi akitaka Lyimo athibitishe au afute kauli yake juu ya madai hayo wakati serikali imenunua magari 32.

“Hata kwa akili ya kawaida haiwezekani Serikali ikaagiza magari yote hayo 777 ya washawasha. Ninachokumbuka mimi Waziri huyu aliwahi kusema hapa bungeni kuwa magari hayo 777 ni idadi ya magari yote ya aina mbalimbali yaliyonunuliwa kwa ajili ya matumizi ya polisi,” alisisitiza Ndugai.

“Sasa nakutaka uniandikie rasmi majibu vizuri kuhusu kauli yako hii, nakupa siku tatu uwe umeniletea na baadaye nitaipeleka taarifa yako kwa Kamati ya Maadili ya Bunge, ili kujadili suala hili kwa mapana,”alisisitiza Ndugai.

Awali mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, Ndugai alimpatia mbunge huyo nafasi ya ama kufuta kauli yake hiyo au aithibitishe kabla ya hatua za kikanuni za Bunge hazijachukuliwa dhidi yake.

Lyimo alikataa kufuta kauli hiyo na kudai kuwa anao uthibitisho juu ya idadi hiyo ya magari aliyoitamka na kusisitiza kuwa amenukuu taarifa za idadi hiyo kupitia taarifa iliyotolewa na mtandao wa Jamii forum pamoja na taarifa za Hansad za Bunge.

“Mheshimiwa Spika mimi ni mtu mzima siwezi kwenda kwa hisia za watu, ni kweli jana niliombewa mwongozo bahati mbaya sikuwepo ndani ya Bunge. Nathibitisha kauli yangu na wala siifuti kwa kuwa nina uhakika na idadi ya magari niliyoisema,” alisisitiza mbunge huyo.

Alisema kwa mujibu wa Kanuni ya 63 (2) ya Bunge, mbunge hatasema uongo endapo chochote atakachokisema ndani ya Bunge atakuwa amekirejea kwenye chombo cha habari au taarifa za Bunge.

0 Response to " Mbunge Apewa Siku 3 Atoe Ushahidi wa Magari 777 ya Washawasha"

Post a Comment