Mvulana huyo kwa jina Jani ametunukiwa $10,000 (£7,000) baada ya kugundua udhaifu huo uliowezesha mtu kuingia kwenye mtandao huo wa kusambaza picha na kufuta maoni ya watu.
Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba kisheria haruhusiwi kutumia mtandao huo hadi atimize umri wa miaka 13. Kampuni ya Facebook ambayo inamiliki Instagram, ilichukua hatua upesi na kuondoa udhaifu huo.
Sasa, ndiye mtu mchanga zaidi kutunukiwa pesa kwa kugundua udhaifu katika mitandao ya kampuni hiyo. Aliandikia wasimamizi wa mtandao huo barua pepe Februari kuwafahamisha kuhusu ugunduzi wake.
Wataalamu wa mtandao huo walimfungulia akaunti ndipo aweze kuthibitisha madai yake na akafanikiwa. Mvulana huyo kutoka Helsinki, ameambia gazeti la Iltalehti la Finland kwamba atatumia pesa hizo kununua baiskeli, mpira na mavazi ya kuchezea kandanda na kompyuta za kutumiwa na ndugu zake.
Facebook imeambia BBC kwamba imelipa jumla ya $4.3m kwa watu waliogundua udhaifu kwenye mitandao yake. Malipo hayo hutolewa kama kishawishi kuzuia watu kuuzia wahalifu ugunduzi wao na hivyo kusaidia kampuni husika.
0 Response to "Huu ni Udhaifu wa Instagram Uliogunduliwa na Mtoto wa Miaka 10"
Post a Comment