Mahakama ya Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, imemhukumu kwenda jela miaka 12, Qasama Machibya aliyejifanya ofisa usalama wa Taifa kwenye ziara ya Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete mwaka 2013.
Kabla ya hukumu, mshtakiwa alijitetea mahakamani hapo kuwa kitambulisho alichokutwa nacho siyo chake na anashangaa kuona kuna picha yake na jina lake.
Alidai kuwa hizo ni mbinu za polisi kumminya, hivyo aliiomba Mahakama kumpunguzia adhabu na kwamba ana ugonjwa wa Ukimwi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Gabriel Kurwijila alisema utetezi wa mshtakiwa hauifanyi mahakama kutomtia hatiani kwa kuwa hana cheti cha ugonjwa.
Alisema kutokana na mahakama kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka uliowasilishwa inamtia hatiani kwa makosa matatu.
Kurwijila alisema kosa la kwanza ni kughushi nyaraka ya Serikali hivyo, atakwenda jela miaka mitano na kosa la pili la kujifanya ofisa usalama wa Taifa kifungo chake ni miaka miwili.
Alisema katika kosa la tatu la kuudanganya umma kwa kutoa nyaraka iliyoghushiwa hivyo, atatumikia adhabu gerezani miaka mitano.
Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Elias Mgobela alisema mshtakiwa alikamatwa wakati Kikwete alipokuwa akitarajia kuhutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara.
0 Response to "Aliyejifanya Ofisa usalama wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete Atupwa jela Miaka 12"
Post a Comment